Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ayatullah Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan, amesema kuwa: Kutokana na ukosefu wa uadilifu wa kiuchumi, leo hii ubinadamu duniani kote unateseka chini ya mfumo wa kitabaka.
Amesema kuwa, kutokana na ukosefu wa mazingira na fursa sawa, maskini wamenyimwa hata mahitaji ya msingi ya maisha. Ameongeza kuwa ujamaa na ubepari vimeshindwa kuleta uadilifu wa kiuchumi duniani, na zaidi ya hayo, mfumo huu dhalimu wa kimataifa haujasita kutumia kila mbinu ili kuilea serikali ya Kizayuni.
Ayatullah Sajid Naqvi amesema: Hali ya Gaza ni picha ya kutisha ya ukweli huu; eneo ambalo baada ya mabomu yenye uzito wa maelfu ya tani na marufuku dhidi ya misaada ya kibinadamu, limekumbwa na janga la njaa huku jitihada za kuangamiza ubinadamu zikiendelea.
Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan ameongeza kuwa: Umoja wa Mataifa, ingawa kwa sura ya nje ni taasisi inayokubalika kimataifa na hata kutenga siku maalumu kwa ajili ya uelimishaji wa umma, lakini taasisi hiyo yenye nguvu inahitaji kuchukua hatua za kivitendo. Mfumo wa kiuchumi wa kinyonyaji wa dunia umebanwa mikononi mwa madola dhalimu; ujamaa na ubepari, licha ya kaulimbiu zao zenye mvuto, zimeshindwa kutoa uadilifu wa kiuchumi kwa wanadamu na badala yake zimefanya hali kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Kwa mujibu wa takwimu za zamani za Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 15 ya watu duniani wanateseka kutokana na uhaba wa chakula, jambo ambalo chanzo chake kikuu ni mfumo wa kiuchumi wa kinyonyaji na utawala dhalimu.
Ameongeza kuwa: Uislamu ni mfumo kamili wa maisha ambao ni mtangulizi wa haki sawa, uadilifu wa kiuchumi na utawala wa haki; na mfano bora zaidi wa hayo ni mfumo wa haki wa Imam Ali (a.s) ambao utabaki kuwa kielelezo cha uadilifu na usawa daima.
Ayatullah Sajid Naqvi pia amezungumzia hali ya kiuchumi ya Pakistan akisema: Siku ya Chakula Duniani inasherehekewa wakati nchi ipo katika kipindi cha kuwasilisha bajeti ya mwaka wa kifedha wa serikali kuu huku ikikabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mujibu wa takwimu, takriban watu milioni 20 wa Pakistan wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Bajeti ya sasa ni mkusanyiko wa nambari na takwimu pekee ambazo badala ya kupunguza matatizo ya kiuchumi ya wananchi, zinazidi kuyaongeza; hivyo kunahitajika marekebisho na hatua za haraka.
Your Comment